SA国际传媒

Tafuta

Papa Francisko anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema Jumatatu tarehe 7 Oktoba 2024 kufunga na kusali, kwa ajili ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia. Papa Francisko anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema Jumatatu tarehe 7 Oktoba 2024 kufunga na kusali, kwa ajili ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia.   (AFP or licensors)

Papa Francisko: Tarehe 7 Oktoba 2024 Siku ya Toba, Kusali na Kufunga!

Papa Francisko anawaalika Mababa wa Sinodi, waamini na watu wote wenye mapenzi mema Jumatatu tarehe 7 Oktoba 2024 kufunga na kusali, kwa ajili ya kuombea duniani. Dominika tarehe 6 Oktoba 2024 majira ya Saa 1:00 za Usiku atakwenda kusali Rozari kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Roma, ili kuombea amani na upatanisho. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, tayari limeitikia wito huu wa Baba Mtakatifu Francisko na watu wa Mungu watajiunga kusali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane wa XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Pacen in terris” yaani “Kuhusu kuimarisha amani kati ya watu wote katika ukweli, haki, upendo na uhuru anasema amani duniani, ambayo watu wa nyakati zote waliitamani kwa hamu kubwa sana, haiwezi kujengwa wala kuimarishwa isipokuwa kwa kulinda kitakatifu utaratibu uliowekwa na Mwenyezi Mungu. Kwa njia ya maendeleo ya sayansi mbalimbali na vumbuzi za teknolojia mpya, mwanadamu amefahamu zaidi kwamba utaratibu wa ajabu unafanya kazi katika viumbe na katika nguvu za asili, na kwamba, uliyoipokea mtu ana cheo maalum, kiasi cha kuweza kutambua utaratibu huo na kutengeneza nyenzo ili kutawala nguvu hizi na kuzigeuza ziwe kwa manufaa yake. Maendeleo makubwa ya sayansi na uvumbuzi wa kiteknolojia unadhihirisha ukuu wa Mungu usiokuwa na mipaka. Rej. Pacem in terris, 1.

Papa Dominika 6 Oktoba 2024 Sala ya Rozari Kuombea Amani
Papa Dominika 6 Oktoba 2024 Sala ya Rozari Kuombea Amani

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika kwanza Mababa wa Sinodi, waamini na watu wote wenye mapenzi mema Jumatatu tarehe 7 Oktoba 2024 kufanya toba, kufunga na kusali, kwa ajili ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia. Dominika tarehe 6 Oktoba 2024 majira ya Saa 1:00 za Usiku atakwenda kusali Rozari Takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Roma, ili kuombea amani na upatanisho. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, tayari limeitikia wito huu wa Baba Mtakatifu Francisko na watu wa Mungu watajiunga kusali Rozari na Baba Mtakatifu na hatimaye, kufunga na kusali, Jumatatu tarehe 7 Oktoba 2024. Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI anasema, kila siku kuna ongezeko la athari za vita sehemu mbalimbali za dunia. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi, kutochoka kuomba huruma na msaada wa Mungu ili hatimaye, amani iweze kupatikana. Chuki na uhasama viache nafasi kwa haki, amani na upendo; utengano utoe nafsi kwa umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Huu ni wakati muafaka wa kusitisha vita na kwamba, kila mtu asimame kidete kutekeleza dhamana na wajibu wake, kwa kutambua kwamba, kila mtu anapaswa kuwa ni shuhuda na mjenzi wa amani.

Vita inaendeleaq kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao
Vita inaendeleaq kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao

Kuhusu Kufunga: Awali ya yote Kristo Yesu alipigania kupata ushindi, lakini siyo kwa ajili yake, bali kwa ajili ya kutufundisha jinsi ya kupigana. Hata Yesu mwenyewe alifunga na kutoa kipaumbele katika mfungo ili kuvivunja vifungo vya mshawishi Shetani, Ibilisi. Kwa hiyo mapambano yetu ya kuombea amani ni kufunga. Mtakatifu Ambrosi anasema: “Mfungo una nguvu ya ajabu kwa sababu hata Kristo Yesu mwenyewe alifunga. Mfungo ni mzuri kwa sababu humwinua binadamu na kumpeleka hadi juu mbinguni. Mfungo ni zoezi mwafaka la kukarabati roho na mwili. Mfungo ni chakula cha kiroho, ni maisha ya kimalaika, ni kifo cha dhambi, mwisho wa uhalifu, ni njia ya ukombozi, ni chanzo cha neema, baraka na msingi wa usafi wa moyo.” Kwa hiyo yatubidi tutambue kuwa mfungo ni nidhamu inayotakiwa kufuatwa na watu wote kwa manufaa ya jamii. Yaani kufunga kwa ajili ya kuombea amani. Kadhalika kufunga kwa ajili ya kuombea ulimwengu uliojaa matatizo na kukithiri maovu ya kila aina. Kwa hiyo, faida kuu ya mfungo kijamii unayo maana sana tena inayolenga kukuza na kudumisha hadhi ya binadamu. Mfungo huu utusaidie kutenga muda kwa ajili ya Sala na tafakari ya Neno la Mungu. Kwa kufanya hivyo, watu polepole watagundua jinsi ya kujenga nidhamu ya maisha ya kiroho ambayo ni fursa mwafaka kwa maisha ya kiroho.  Lengo kuu kwetu sisi sote pamoja na Kanisa zima ni kusafiri na Bikira Maria kumwendea Kristo Yesu, Mfalme wa amani, ili aweze kutukirimia amani ya kudumu.

Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu
Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu

Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala anasema Sala ni chemchemi ya imani na kilio kinachobubujika kutoka katika undani wa mwamini kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu.  Ameendelea kujikita katika: Sala na Utatu Mtakatifu kwa kujielekeza zaidi kwa Roho Mtakatifu anayewafunulia watu kumhusu Kristo Yesu. Roho Mtakatifu anao uwezo wa kuchunguza hata Mafumbo ya Mungu. Ni Mungu peke yake anayemjua Mungu kabisa. Kanisa linamsadiki Roho Mtakatifu kwa sababu ni Mungu na kamwe haliachi kutangaza imani kwa Mungu mmoja: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kanisa ni Mama, Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala na kwamba, kuna mitindo mbalimbali ya sala, ili kuweza kuzungumza na Mwenyezi Mungu: Sala ya Sauti, Sala Fikara au Tafakari na Taamuli.

Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu
Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu

Baba Mtakatifu amegusia kuhusu umuhimu wa utume wa sala na changamoto zake. Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri zaidi. Kanisa ni shule kuu ya sala. Kristo Yesu ni njia ya kwenda kwa Baba wa mbinguni na kabla ya kupaa kwake kwenda mbinguni aliwaahidia kwamba, atawaombea kwa Baba yake wa mbinguni ili kwa jina lake awaletee Roho Mtakatifu na Roho wa kweli atakaye kaa pamoja nao milele yote. Roho Mtakatifu atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote walioambiwa na Kristo Yesu alipokuwa angali kati yao! Rej. Yn. 14: 25-26; 16:12-15. Kristo Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba, bado alikuwa na mambo mengi ya kuwaambia. “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari.” Yn. 16:13-15. Sala kama Tafakari kwa Mkristo ni muhtasari wa Ufunuo wa Mungu unaonafsishwa katika maisha ya mwamini. Mababa wa Kanisa wanasema, kutafakari kile ambacho mtu anasoma humwongoza kukifanya kuwa chake kwa kukipambanisha na yeye mwenyewe. Hapa kitabu kingine kinafunguliwa: kile cha maisha. Mtu hupitia mawazo kufikia ukweli. Kadiri ya kipimo cha unyenyekevu na imani mtu hugundua mienendo inayoamsha moyo na anaweza kujipambanua. Rej. KKK. 2706.

Vita inasababisha mateso na mahangaiko kwa watu wa Mungu
Vita inasababisha mateso na mahangaiko kwa watu wa Mungu

Ikumbukwe kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 7 Septemba 2013 katika mkesha wa kuzaliwa kwa Bikira Maria, Malkia wa amani, aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Siria na, Mashariki ya Kati na Ulimwengu katika ujumla wake, kwa sababu vita ni chanzo kikuu cha maafa. Tarehe 23 Februari 2018, Ijumaa ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima, Baba Mtakatifu Francisko akatoa mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kufunga kwa ajili ya kuombea amani Sudan ya Kusini na DRC, ili watu wa Mungu waweze kujikita katika ujenzi wa amani ambayo ni kwa mafao ya wengi. Tarehe 4 Septemba 2020, Baba Mtakatifu aliitisha Siku maalum ya kusali na kufunga kwa ajili amani na mshikamano nchini Lebanon. Tarehe 29 Agosti 2021 Baba Mtakatifu alitoa mwaliko wa kusali, kufunga, ili kumwomba Mungu awezeshe majadiliano, mshikamano na upendo nchini Afghanstan. Tarehe 2 Machi 2022 mwanzo wa vita kati ya Urusi na Ukraine, akaitisha siku ya sala na kufunga, ili kuombea amani nchini Ukraine. Tarehe 27 Oktoba 2023, Kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mtakatifu Yohane XXIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Pacen in terris” yaani “Kuhusu kuimarisha amani kati ya watu wote katika ukweli, haki, upendo na uhuru aliitisha siku maalum ya kufunga, kusali; toba na upatanisho, ili kuombea mchakato wa upatanisho ulimwenguni.

Sala na Kufunga
04 October 2024, 14:52