SA国际传媒

Tafuta

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari Dominika 27 ya Mwaka B wa Kanisa: Tunu Msingi za Familia

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Kwa neema ya Mungu tupo dominika ya 27 ya mwaka B, na leo kipekee tunatafakari ya taasisi msingi sana yaani familia inayozaliwa katika sakramenti ya ndoa, tangu kuumbwa kwa mwanadamu Mungu aliona hili kuwa kwa kiumbe wake hasa katika kuitiisha dunia na kuuchuchumilia ukamilifu, katika kuitimsiha kazi uumbaji akasema, Kisha kuumba mbingu na dunia Mungu aliona kila kitu alichokifanya ni chema sana (Mwz 1:31). Kitu cha kwanza kibaya kutajwa na Mungu Mwenyewe kabla hata dhambi haijaingia duniani ni upweke, ‘si vema mtu huyo awe peke yake…’ Upweke huondoka kwa kuwa na wenzetu walio tayari kutusikiliza na kutufariji, ndipo umuhimu wa maisha ya jumuiya unapojitokeza… Upweke wa kindoa huweza kumuathiri mmoja hivi akajikuta hana analofaulu katika vipengele vyote vya maisha yake. Ndoa ni agano ambalo kwalo mwanamume na mwanamke huunda kati yao jumuiya kwa maisha yote. Agano hili ni kwa ajili yao na kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Linafungwa baina ya wabatizwa, nalo limeinuliwa na Kristo Bwana kwa hadhi ya Sakramenti (Kan. 1055#1, KKK 1601). Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Dumisheni tunu msingi za maisha ya ndoa na familia
Dumisheni tunu msingi za maisha ya ndoa na familia

UFAFANUZI: Thamani ya Ndoa inaanzia kwenye Maandiko Matakatifu. Pazia la Biblia hufunguliwa na uumbaji wa mwanamume na mwanamke, kuwabariki na kuwapa amri na uwezo wa uzazi (Mwz 1:27-28) na humalizika na maono ya harusi ya Mwanakondoo “alleluia, wakati wa harusi ya mwanakondoo umefika, na bibi harusi yupo tayari alleluia” (Ufu 19:9). Thamani ya ndoa inajidhihirisha kwenye dhana ya familia ambapo msingi wake upo katika chaguo la hiari la wawili kuunganika kwa hiyo taasisi hii ya ndoa ni uhusiano wa ndani wa kimaisha na wa kimapendo uliowekwa na Muumba na Yeye mwenyewe akaiwekea sheria zilizo sahihi anavyoelekeza Kristo katika Injili ya leo (Mk 10:2-16)... Katika Ndoa wawili wanajuana na kupokeana na kisha kujitoa mmoja kwa mwingine wakikamilishana kwa tendo la upendo wa kindoa ambalo ni zawadi kamili na timilifu ya mtu kwa mtu isiyoweza kufananishwa na chochote. Thamani ya Ndoa inanogeshwa na ukweli kwamba Ndoa ni sakramenti iliyo ishara na chombo cha neema ikifafanua maana ya ushirika wa kimapendo kati ya Mungu na wanadamu ambayo imekuwepo wakati wote wa historia ya ukombozi. Ndoa ni kifungo cha ajabu tena ni fumbo ambalo kwalo muungano wa kimapendo wa Kristo na Kanisa unadhihirishwa kwa ishara ya muungano wa mume na mke (Efe 5:21-33). Hivi wanandoa, katika umoja wao wa kimwili, kiakili na kiroho wanakuwa ishara safi ya Kristo Bwana harusi na Mama Kanisa bibi harusi.

Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo
Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo

Thamani wa kifungo hiki unaonekana pia katika kuwapa mume na mke uwezo na uwajibikaji katika kuishi wito wao kama walei na kwa njia hiyo kuutafuta ufalme wa Mungu kwa kujihusisha na mambo ya kidunia na kuyaweka katika utaratibu kulingana na mpango wa Mungu.  Kwa hiyo ndoa inaunganika na Kanisa kwa fadhila ya sakramenti inayoifanya iwe “Kanisa la nyumbani”. Kwa kuzingatia ‘uthamani mkubwa wa Ndoa takatifu’ wenye wito huu watambue Ndoa sio jambo dogo au kitu tu chepesi. Watunze usafi wa sakramenti ili wafaidi neema zake. Wawe mashahidi katika kutangaza maana ya ndoa ambayo jamii ya sasa imefikia hali ngumu sana kuweza kuitambua... wazingatie mashauri ya Injili, wapendane na kujisadaka ikibidi kufa kwa ajili ya mwingine (Yn 15:13), kwa njia hii huhubiri wakiwavutia wengi kwa Kristo. Ni matashi ya Mungu kadiri ya somo I (Mwz 2:18-24) wahusiane katika usaidizi mwema na wa kufanana, uhusiano usiwe wa Bwana na mjakazi, bosi na mtumwa, simba na swala bali uwe ni wa kimapendo. Mungu alimpa Adamu mke kutoka ubavuni mwake. Kilichotumiwa kumfanya Eva hakikutolewa miguuni, Adamu angefikiri kumshusha thamani na kumfanya mtumwa miguuni pake. Kadhalika hakikutolewa kichwani, Eva angempanda Adam kichwani na kujipa mamlaka. Mwanamke alitoka ubavuni karibu na moyo, maskani ya upendo, apate kusimama naye kama mwenzi sawa na yeye, basi “ndoa na iheshimiwe na watu wote na malezi yawe safi” (Ebr 13:4a).

Familia ni kitovu cha maisha ya kijamii
Familia ni kitovu cha maisha ya kijamii

Pamoja na kuwa imara kiroho, wanandoa wakumbuke mtu ni mwili pia wenye mahitaji, hayo hupatikana kwa mipango ya pamoja ya maendeleo na utekelezaji wake. Mwanadamu huwa na utulivu anapokuwa na hakika ya kesho akitambua chakula kipo, watoto wanasoma, anaweza kutibiwa, kusafiri na kutimiza ndoto zake. Hili linadai uchapakazi, wepesi na subira. Uvivu ndio chanzo cha ugomvi katika familia, unashusha hadhi na kukupoteza heshima. Mungu atakapobariki juhudi zetu na kutuneemesha tutumie mapaji hayo kwa ajili ya kuueneza ufalme wake, tutakamilika tukifurahia yote katika pendo lake Kristo. Leo Kristo anapokazia utakatifu, uimara na thamani ya Ndoa (Mk 10:2-16) tunawaombea akina baba wawe waume wema. Sifa za mume mwema 1. mcha Mungu 2. anampenda mke wake kama nafsi yake. 3. ana uwezo wa kuiongoza familia yake 4. mwenye kuihudumia familia yake 5. mwenye kuwafundisha watoto njia inayopasa 6. anamuheshimu mkewe 7. Kuhani wa familia 8. Mnadhimu anayehakikisha nidhamu na ulinzi wa nyumba yake… Nampenda Baba mwenye uwezo wa kusema “chagueni hivi leo mtakayemtumikia lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana” (Yosh 24:15).

Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo
Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo

Halafu tunawaombea mama zetu wawe wake wema… “Mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake, bali mpumbavu huibomoa nyumba yake...kwa mikono yake mwenyewe” (Mith 14:1). Mke mwema… 1. Si mtu wa kulalamika na kunung’unika 2. ana kiasi, hana madai mengi mume asije iba ili amfurahishe. 3. humuheshimu mumewe kwa mawazo na kwa matendo akimshauri mambo mema 4. humtii Mungu katika vipengele vyote vya maisha yake 5. humtii mumewe na kupokea maongozi yake 6. anajitahidi kushika na kufuata mashauri ya kimungu 7. hajidanganyi kumtawala mumewe na kujiona kuwa unajua zaidi yake 8. Si mvivu 9. Kwake daima ni Mungu kwanza. Maisha ya ndoa ni safari… barabara ya mafanikio kimwili na kiroho sio pana na sio nyoofu, ina vidhibiti mwendo vingi viitwavyo MAADUI, kona nyingi ziitwazo MAJARIBU, taa za barabarani ziitwazo CHUKI, miteremko mikali ndio MANENO YA WATU, na milima mirefu maarufu kama KUCHOKANA.

Familia ni kitovu cha uinjilishaji
Familia ni kitovu cha uinjilishaji

Mnaposafiri katika njia ya namna hii, pandeni gari moja tu yaani MALENGO NA MATARAJIO, gari hili lina injini ya kisasa na mpya iitwayo KANISA yenye mwendo kasi kubwa kabisa, tumieni leseni ya udereva iitwayo IMANI, aendeshe dereva mmoja tu KRISTO naye atawaafikisheni salama salimini kwenye hiyo nyumba ya MAFANIKIO hapa duniani na baadaye katika Ufalme wa mbinguni… Wajenge nyumba ya URAFIKI kwa gharama ya MAPENDO, muwaajili mafundi stadi kutoka MOYONI, vibarua wachapakazi kutoka NAFSINI, mkitumia mchanga wa UMOJA, udongo wa MATUMAINI, milango ya HERI, madirisha ya WEMA, vitasa vya HEKIMA na kufuri za BUSARA, nyumba yenu iezekwe kwa mabati ya NIA NJEMA na muizungushie fence/ukuta wa DAMU YA YESU. Tutakiane baraka tukiombeana neema ya kuishi kwa amani, kuamua kwa busara, kutenda kwa hekima, kupenda kwa dhati, kuomba kwa imani, kuhubiri kwa matendo, kuongea kwa nidhamu, kutii kwa unyenyekevu, kuabudu katika roho na kweli, kutenda kwa wakati, kujitathmini tumetoka wapi, tupo wapi na wapi tunaelekea kimwili, kiroho na kimaendeleo. Zaidi ya yote tujiheshimu, tujitunze na tujitafakari kwani vyote vinatokana na jinsi tulivyo wenyewe naye Mungu yu pamoja nasi sasa na hata milele. BWANA na atubariki atulinde na kutuhifadhi, amina.

Liturujia D 27
04 October 2024, 13:55